Asiye na wake aelekee jiwe. Jane Leperet Maiyan alikuwa amekata tamaa kabisa kwamba Josephat Ole Meripet atakuwa wake. Akipatana naye anamsalimia kwa heshima, anarembua macho, anacheka cheka na kumguza guza mabega ilimradi ajionee kuwa amemteka mawazo. Lakini wapi. Josephat hakupania kuyaona hayo. Jane akashikwa na hamaki na hatimaye akamuitisha nambari ya simu. Akawa anamtumia jumbe fupi fupi za utani Whatsapp, huku akimuuliza tumaswali twa kumsoma kama ana hisia za kimapenzi kwake. Puuuuu. Hakuna alama wala dalili yoyote ya kumpa Jane afueni na kumuondolea dukuduku moyoni. Ama anaringa?? Kwani anajiona aje asali?? Niachane na yeye?? Jane alijiuliza maswali chungu mnzima. Kwa kweli alikwishampenda Josephat, lakini akimuambia waziwazi, atamuona kahaba ama changundoa.
Siku ya kwanza Jane kumuona Josephat alizubaa, hadi akateguka na kuanguka. Kidogo avunjike ulimi. Alikuwa ametoka kumsalimia rafikiye Mary aliyeishi dakika chache kutoka nyumbani kwao. Josephat alikuwa mgeni jijini Narok baada ya kuletwa huku kikazi katika Supermarket ya Quickmart. Tangu hiyo siku, Jane alijiambia kimoyomoyo “huyu ndiye atakayenioa, la sivyo nitajiunga na kanisa nisioleke wala kuzaa”.
…CONTINUE READING